Wakati
2023-06-15
Maelezo
I: na picha nyingine, picha hii imesajiliw kwa namba 2018_18555_001, hebu angalia picha hiyo, unaweza ukatambua hiki ni kitu gani
R: huu kwa waswahili wanasema ''mtemba' lakini sisi tunaita 'kiko'...
I: kiko ni lugha gani
R: ni kisambaa
I: na mtemba
R: mtemba ni kiswahili ambacho watu wanachukua tumbaku wanaweka kwenye mtemba, basi mtu mwenyewe akiwa kule anavuta
I: kwa hiyo kisambaa ni kiko
R: kiko ee, mtu anakuambia kaniletee kiko changu, yani kanilete mtemba wangu, halafu na mkaa na uulete ule mkaa vizuri akija anaweka kiko lake hapo, basi yeye mwenyewe amekaa huku kando haswa haswa majumbe ndio wanavuta, akimaliza anakung'uta hata kama ni sehemu ukikaa karibu anaweza akakukung’utia halafu anakuambia nenda ukaondoe hilo jivu lote tena unaanza tena, lakin kwa sasa hivi wanaitengeneza lakini sio kama ya zamani, hii ya zamani iko still sana yaani ni mizuri mno
I: ni majumbe tu ndio walikuwa wakivuta
R: ni watu maarufu ambao wanavuta, wadoe wanavuta lakini mbele ya jumbe huwezi ukavuta mtemba kama ule, labda nyumbani mwako na wake zako, lakini umekaa na jumbe uvute huo, anakumbia huyu ni nani anayetuiga sisi …oh...
Wote: wanacheka
R: hasa baba yake yule mkande, baba yake alikuwa 'ushe ni ndai we' yani ‘huyu anayetaka kutuchukua milki ni nani’, huyo, na wewe pia huwezi unaogopa kwenda kubanwa au kwenda kuwekwa sehemu ambayo ni mbaya kwa ajili ya kuvuta mtemba au tunaita kiko
I: mitemba ilikuwa inavutwa na watu wa makabila gani hasa
R: ni watu wenye nafasi tu
I: unaweza ukawatambua kwa makabila yao
R: sana sana wasambaa, wambugu, wazigua wanapenda sana mambo ya ufalme ufalme, na wenzetu wazigua unamkuta mtu ana nyumba zaidi ya nne, akikuambia kaniletee mtemba wangu kwenye nyumba ndogo basi ukimkuta hapo amekaa hapo nje amekaa kwenye kiti chake, kuna viti vile ambavyo ni vya magunia, basi mtu amekaa anavuta, ukivuta hiyo ni mtu mmoja marufu sana
I: na ni mikoa gani hasa kiko na mitemba ilikuwa ikipatikana
R: sana sana tanga ndio inapatikana, lakini sana sana mikoa ya bara na uziguani huko, wazigua wanajua sana mambo ya utamaduni sana, wazigua wanapenda sana utamaduni huo, hata viti hivi ambavyo nimeviona, kuna viti kama vya kupigia ngoma kama ile ya mzee chei ambayo ikipigwa kama kuna jambo la ajali au maradhi inamjulisha basi ile ngoma inalia tu yenyewe 'ndi ndi ndi', basi kwenye mikoa ambayo wanapenda sana huu utamaduni ni uziguani huko na hapa kazita pia ambapo ni Handei, ambapo hapa zamani waliita amani-handei
I: na ni wazee wa umri gani walikuwa wakivuta kiko
R: ni mpaka uruhusiwe, ukishaoa ndio unaruhusiwa uvute kiko
I: kwa hiyo walikuwa ni kuanzia miaka mingapi
R: kuanzia… yaani wewe tu unaenda uchungaji ukija unarudi unanyonya kwa mama yako, ni uwe na miaka 30, 35 ndio unapewa, na huyo mke ni wa kupewa uende kwenye nyumba ya fulani ndio ukaoe, na pia ukipewa huu mtemba mpaka uukomboe labda kwa babu yako ndio uuvute
I: unaukomboa kwa namna gani
R: labda umekwenda kumlimia ungwe au kama umempa hela 5 ndio anakumbia sasa ninakuruhusu tumbaku uvute, lakini huwezi ukavuta kama sasa hivi mtu hajamaliza hata darasa la 4 anavuta, zamani ni mpaka uruhusiwe na babu, sio baba yako ni babu, anajua sasa huyu ana mji wake, ana nyumba yake na familia yake ndio anakuruhusu sasa, lakini sasa hivi...
Wote: wanacheka
R: ah, ni mambo ya kale, yani haya yananikumbusha mambo ya zamani sana
I: wanawake walikuwa wakivuta mitemba
R: hamna
I: kwa nini
R: wanawake walikuwa wanachukua sigara ten cent na magadi anaweka hapa, lakini humkuti mwanamke anavuta
I: kwa nini wanawake walikuwa hawavuti mitemba
R: wanawake walikuwa kweli walikuwa wanaonelewa sana, yani mwanamke hawezi akapewa uhuru, na sana sana yeye ataambiwa niletee mtembo wangu hapo, niletee kiko changu hapo, kiko karibu na kitanda, na hawezi akagusa na yeye akafanya 'fuu' apulizie mwenyewe avute ndio kinakolea huku, anakuambia sana sana njoo uchukue ukatupe majivu halafu tena uniongezee tumbaku
I: kwa hiyo wao walikuwa wakitumikishwa
R: walikuwa wakitumikishwa tu, hawezi akaruhusiwa kuvuta
I: na kiko kwa sasa vinatumika au unadhani vimepotea havina thamani tena katika jamii
R: mimi hilo umenikumbusha nina miaka sio chini ya 50 kukiona hiki, niliokota kiko huku mashambani kama hiki kidogo lakini sasa hivi sijaona, sijui kwenye maduka au wamasai wamasai wanaweza wakatengeneza vitu vya utamaduni, lakini kwa sasa hivi huku hakuna na wala nisikudanganye
I: umesema hiyo inaendana na tumbaku na mkaa wa moto, na anayevuta umesema anakuwa kwenye kiti maalum, unaweza kutuambia kiti hiki kinakuwaje
R: kuna vile viti kama vya magunia vinajikunja vyenyewe, anakunjua halafu anakaa, analala ni kama kitanda lakini sio kitanda...
I: ni vile viti vya uvivu wanasema
R: ee wanasema viti vya uvivu, hapo basi ukimkuta amekaa hapo, kimbia uondoke uende uchungaji atakutuma kiko tu...
Wote: wanacheka
R: ukishamuona ametoka nje amekaa hapo na fimbo yake lazima atakuambia, 'hei njoo, kalete kiko', na moto labda hauko pale utatafuta hata nyumba nyingine
I: na kilikuwa kuna umuhimu gani kwa utamaduni wa watu uliowataja
R: ilikuwa ni kama hawa vijana wa sasa hivi wanaovuta sigara, na mimi mwenyewe pia nimevuta sigara, yani ni kama kinaleta hisia kama kufikiri
I: ulisema kuwa vijana walikuwa wanaruhusiwa na babu, ilionekana ilikuwa ni muhimu sana kwenye mswala ya kimila au na kiutamaduni, ilikuwa ina umuhimu gani hasa mpaka inafikia hatua kwamba...
R: hii huwezi ukavuta kama ni kijana, anajua kwamba huyu bwana tayari ana mke na ameshaozeshwa, na ndio maana unamkuta naye ana kiko, ni ishara ya kusema wewe umekomaa, ni sawa sawa na wenzetu wamasai akiozeshwa mke ni mpaka ameua simba, na sisi mila zetu tunasema huyu jamaa sasa hivi hawezekani, nayo ndio hivyo hivyo...
Wote: wanacheka
R: umenielewa hapo, wanasema mradi anavuta kiko huyu amekuwa na nyumba unaiweza na mke wako, manake sio siri zamani tulipokuwa sisi hata muende mkaoge na msichana hujui kwamba ni nini ile, sasa hivi we wanajua, kuna siku moja mimi na jamaa yangu tulikuwa tunakunywa chai tunasoma darasa la 4, unashiria hata huyo mke uliyekuwa naye unammudu ndio unavuta kiko, sasa wewe huna shamba, chakula ni cha kuitiwa na baba yako halafu unavuta sigara, mke wako pia anatunzwa na mama yako na baba yako
I: mzee [anonymous] hebu tuambie, kiko walikuwa wanatengeneza wakina nani, wa jinsia gani ana umri gani
R: wanaotengeneza ni watu wenye umri wa miaka 20 - 25, lakini wewe kijana huwezi ukatengeneza kiko hiki, kwanza utakianzaje, hata hii miti sasa hivi huwezi ukaipata, hii miti ni still, lakini miti ya sasa hivi ukitengeneza kiko ukivuta tu na huu moshi tayari kinaungua, lakini hii miti ni still sana, na huwezi ukaipata
I: unaweza ukatauambia ilikuwa inatengenezwa kwa miti gani.... na hiki ni nini, ni chungungu au ni...
R: hiki ni chungu, walikuwa wanatengeneza vyungu, kuna udongo fulani ambao ni mgumu sana kwa kweli, hata ukitenegeneza vyungu unapikia, sasa hivi unasonga ugali kwenye sufuria lakini zamani ni kwenye chungu, mahindi sasa hivi si ni kukoboa lakini zamamni lazima ufunde halafu unaloweka, ugali wa wake ni mzuri mno, sasa ni udongo ambao sielewi kama sasa hivi udongo upo
I: na huo mti mgumu ulikuwa unaitwaje
R: hii miti kwa kweli nimeisahau majina lakini wanasema ni asili kama mpingo lakini kuna kitu wanatoboa kama tundu, wanachoma kwenye moto wanatoboa
I: na hiyo kamba
R: hii kamba inamsaidia sana sana kwenda kutundika havikai chini
I: na hiyo ni kamba gani
R: hizi ni kama kamba za katani wanasuka au hii minyaa ambapo hata vitanda wanasuka masupato yale, sasa hivi tuna lala kwenye mbao lakini vitanda vyenyewe ni vya supatu, kwa kweli umenikumbusha mengi sana, hasa hii mambo ya kiko na ile miti ya amani
I: na kiko kama hicho sasa hivi kikaletwa, sasa hivi kinaweza kuuzwa kwa shilingi ngapi
R: aah, hiki labda laki moja au laki mbili, kwanza nitakitoa wapi, kukipata kwanza sio rahisi
chanzo: Amani-Stade Project / Amani Field Research 2023 / Interview No. 21
mwandishi: I: Mohamed Seif, R: Anonymous
Mtu
-
National Institute for Medical Research (NIMR)
(Mteja)
-
unknown actor
(wissenschaftlicheR BearbeiterIn)
Mahali