Wakati
2023-06-14
Maelezo
I: Sawa sawa asante, sasa tunaenda kwenye picha nyingine yenye vifaa, hapa nina picha nyingine ambayo imesajiliwa kwa namba 2018_18309_1, hebu angali unaweza ukatambua hiki ni kitu gani
R: Hii ni 'mbuhi' lakini Kiswahili chake tunasema 'kengele', lakini ukija katika kilugha kama ya Kipare 'njugha' ambazo kuna nyingine zinafungwa kwenye miguu akicheza ngoma inaitwa 'mwelema', au wakati mwingine kwenye ng'ombe unaweza ukatengeneza kubwa ukamfunga ng'ombe wako mmoja unayeona anatembea tembea sana, kwa hiyo zikienda huko unaisikia hii inalia unajua ng'ombe wako huko, inatumika hii
I: Sawa, hiyo 'njugha' ilikuwa inatumiwa zaidi na watu wa makabila gani hasa
R: Wapare, wakicheza ngoma, Wasambaa pia walikuwa na ngoma yao inaitwa 'upauu' au 'kajanja'
I: Umesema inatumika kama kengele, lakini pia inatumika kwa wanyama, tutaenda kwenye matumizi yote kwa wanyama na kengele, na umetaja majina tofauti ikitumika kwenye ngoma ina jina lake na ikitumika kwa wanyama ina jina lake, je ikitumika kwa wanyama inaitwaje
R: Mmanga'
I: Hiyo ni lugha gani
R: Ni Kipare
I: Hapo ni kwa wanyama na je ukienda kwenye ngoma
R: Njugha, haziwi kubwa ni ndogo ndogo zinakuwa nyingi zinafungwa miguuni ukipiga hivi zinalia na utamu wake na ngoma inapigwa
I: Na hizi njugha zilikuwa zinazalishwa na kusambazwa katika mikoa gani hasa
R: Hizi zilikuwa zinazalishwa hasa kule Upare sehemu moja inaitwa Vudee Nyika na Gonja Maore, kuna sehemu inaitwa Gonja Miamba, huko ndio zilikuwa sasa Kipare wanasema; 'Jishanwa' yani zinatengenezwa ndio utakuta hiyo mivuri ninayowambia wanaita 'kuvugutha' yani ndio unapuliza, lakini hupulizi na mdomo ukifanya 'fuu' unatakiwa utoe kondoo upozwe vinginevyo utajaa tumbo
I: Na kifaa hiki kilikuwa kinatumiwa zaidi na watu wa jinsia gani na wa umri
R: Vijana wanaandaliwa wenye nguvu wenye kuweza kucheza hiyo ngoma
I: Tuanzie kwenye hicho kinachooneka maana hiki kinaonekana ni cha kushika kwa mkono
R: Hiki cha kushika kwa mkono, ngoma zikipigwa sasa watu si wamekaa wamezunguka hivi ni moja ya kwamba ni silaha ya kupiga unashika wewe na kuna anayepiga makopo hivi, kwa hiyo unapata ladha fulani ya ile ngoma yenyewe kupitia vitu hivi, lakini pia hiyo ngoma inayokuwa na hiki imeshikwa inapigwa hivi imekaa wazee wakubwa hapo ujue kuna jambo la kujadili mambo haya mawili, sasa walikuwa wanataka wajadili kuhusu soko, masoko ya zamani yalikuwa hayawekwi kama sasa hii tunavyosema 'nendeni pale ofisini kuna uwanja mkapange vyombo' hakuna hiyo, wazee walikuwa wanaenda na vitu kama hivi siku tatu au nne wanakutana pale, lakini wanaitana kama kitongoji chetu kina vijiji vinne, basi anaitwa mzee wa kitongoji cha cha kwanza, cha pili, cha tatu mpaka cha nne wanakuja wanakaa hapa na hivi vifaa, na watu wanaopiga hizi ngoma na tumbaku zao kwenye vile viko virefu lakini kwa Kipare vinaitwa 'vipunde', wamekaa wanavuta, wanasokota pale anaweka tumbaku halafu wanaanza sasa, hiki kinapigwa na ngoma zinapigwa wanajadili hapo, siku watakayosema kawekeni soko, hilo soko halifi na hakutatokea ugomvi au wizi kwenye hiko soko, lakini sasa hivi masoko yanawekwa watu wanapigana humo sokoni, kwa hiyo inakuwa hali kama hiyo
I: 'Kipunde'
R: Ni kile kiko kirefu, ambacho kiti chake ni viti vya matendegu matatu vinaitwa ‘vichumbi’ ndio wanakaa hao wazee
I: Wazee wa kuanzia umri gani
R: Ni kuanzia miaka 70, 80 na kuendelea, lakini lazima kuna mmoja anaitwa 'mfumwambaha' huyu atakuwa amewazidi wenzie na vitu vingine, yani huyu ndio anayetanguliza kiti kinatangulia kinaenda wekwa anakaa hapo katikati, hata hiyo tumbaku kwenye hicho kipunde inawekwa na wenzie, inawashwa pale yeye kazi yake ni kuvuta tu, akiona anataka kupumzika ananyoosha hivi kuna vijana wako pale wanachukua wanakaa nacho, hilo soko litasimikwa hivyo na halitaleta matatizo
I: Kwa hiyo ilikuwa ni kama sehemu ya tambiko fulani...
R: Lakini kupitia vitu kama hivyo, tuseme sasa hivi tumezoea kusema ni ala za mziki
I: Lakini hiyo ilikuwa inapigwa kwenye ngoma maalum za matukio makubwa kama haya
R: Ee, hizi njugha ni wakati wa kuvuna, wakati kuna sherehe ya kuolewa, ama kuna mgeni anakuja wameandaliwa sasa bwana mkubwa akija awaone ndio wanapiga hizo, lakini hii inapigwa kwenye kitu maalum, aidha ni tambiko la mvua imeleta shida wanakaa wanavitu kama hivi, halafu wakimaliza hapo wanasehemu wanaenda, kwenye msitu wetu huu kuna sehemu tunaita 'wina wamuungu' kwenye huo msitu wetu wa Handei, kuna shimo ambalo tunasema 'wina wa mungu' ukifika limezungukwa na miti mingi
I: Wina wa Mungu manayake ni nini
R: Ni shimo ambalo limekutwa limechimbwa na aliyechimba hajulikani, na wale wakienda huko wanaenda na vitu kama hivyo, halafu hapo hapo kwenye msitu wetu kuna sehemu inaitwa 'kungukaaghe', maana yake ni mtu amehalifu huku, jumbe ameamua kwamba huyu akapotezwe huko kwenye hilo jabali, yani 'kaage', unafungwa huku unapelekwa ukifika pale askari anaitwa 'tarishi' amepewa kirungu anapata hiki mpaka huko chini, hutoki unakwenda kufa huko wanarudi
I: Sawa sawa hapo tumepata majibu ya maswali ambayo yalikuwa yanafuata, hiyo njugha ilikuwa ina umuhimu gani katika tamaduni za Kipare
R: Ilikuwa ina umuhimu kwanza wa kupamba, pili kuboresha, tatu ionekane hasa hata mtu akija...kwanza vile walivyovaa huku juu kuna manyoya ya mbuni, halafu ile kofia yake ni kofia ya ngozi ya mbega, na humu amefunga ngozi nyingine labda ya chui, ukimkuta sasa amevaa ile na akipiga ile miguu namna hii, wewe kwanza kama mgeni unatishika na huwezi kuingia ingia hovyo kule kama hujakaribishwa, utaulizwa umefuata nini na unaweza ukapigwa hata faini, utoe kondoo au uambiwe vinginevyo utakufa, utoe kondoo watu wachinje wale ndio uambiwe nenda sasa hutakufa
I: Na kwa muktadha wa sasa hivi njugha unadhani bado zitaendelea kuhitajika na kutumika kwa tamaduni za watu wa Kipare
R: Ah, sasa ni aghalabu sana, kwa sababu kwanza wazee waliokuwa wanapiga zile wengi wamekufa na watoto wengi wamekataa kuchukua hizo mila, mimi nina ndugu yangu yeye ni daktari wa kupiga oparesheni, lakini baba yangu shangazi yeye ni mganga wa kienyeji, akasema bwana mimi ninakuita ninakaribia kufa kamuita ampe hivi njugha, na tunguri na pembe 'luhembe' ndio hiyo pembe 'luhembe lwa mbala' yani zile pembe za pongo, Kisambaa wanaita 'kuungu' ndio ile pongo, sasa yule ndugu yangu akaitwa kwamba bwana mimi ninaumwa lakini kila nikipima vitu vyangu muda wangu umeenda na njozi zangu zimesema wewe ndio uchukue, akasema baba mimi nimesoma, angalia hizi nguo nilizovaa, wapi na wapi mzee nianze kushika tunguri, sasa ni heri uniambie kitu kingine hiyo mzee utanisamehe kwa sababu umenipeleka shule mwenyewe, akasema nimesema njozi zangu na maono yangu yote ni wewe, akasema mzee hiyo haitawezekana, tena asante baba naenda maana nimeacha wagonjwa kule nitafukuzwa kazi bure, akaondoka akaenda, akasema baba nimekuambia muda wangu ni mchache ila utarudi, alipoondoka kufika nyumbani ilikuja kunguru ikakaa hapa kwenye bega, akienda ofisini kunguru iko hapa, akiingia chooni kunguru iko hapa, akienda kuoga kunguru inakaa hapo mlangoni akitoka kwenye bega, amekwenda nayo hivyo akawa jasiri akasema ah, kwanza wazungu wanapenda ndege wacha ikae tu hapo, kwanza haininyei inakaa inazunguka zunguka, akakaa nayo lakini mwisho wa yote katafutwa na wazee akaambiwa unajua utapata matatizo rudi kwa yule bwana, akaenda na mwisho akamwambia baba nimekubali kuchukua hivyo vitu, akaambiwa tena sasa ndio umeruhusu nife, kwa hiyo ita wazee fulani na fulani, wakaitwa akasema huyu mtu alinikosea lakini kwa sababu amerudi tafuteni kuku, ikatafutwa kuku nyeusi. ni kuku ile yenye manyoya mengi ya kinyafu, akaambiwa waite wenzako wasimame hapo, wakaitwa wakasimama, ile kuku ikichinjwa inaachiwa inapiga 'pupupu' inarudi inakuja malizikia pale kwenye miguu yake akaambiwa ndio yale matamshi yangu, ikakatwa ile nyingine inazunguka kwa wale wote inakuja inamalizikia pale kwenye miguu yake, akasema basi baba mimi nimekubali kuuchukua, kuangalia hivi kunguru haipo na yule mzee akamwambia muda wa kukufundisha sina sasa maana muda wangu umeisha, ila hivi vitu utavitambua kupitia njozi, akawa ni mganga anaagua…
I: Akaacha udaktari
R: Hapana, akitoka kwenye udaktari akija huku nyumbani kuna watu wamekuja wanasema ninashida ya dawa ya chango anampa anaenda, kwa hiyo ilikuwa hivyo, lakini sasa hivi hakuna hivyo vitu kwanza wale wazee wamekufa hawapo, huyo mwenyekiti wetu wa kijiji alikuwa na baba yake hapo, ng'ombe za mzungu zilikuwa zikichinjwa, ikileta tabu anaitwa yule mzee, yule mzee akija ile si ni kali, maana zilikuwa ng'ombe ni za wazungu hapo inachinjwa wanapewa nyama kwa vitu vinaitwa noma, vipande vidogo vidogo unapewa hicho unaenda kuchukua nyama, yule mzee anaipiga kibao, anaipiga huku ng'ombe inaanguka chini kibao kimoja tu, anasema kuleni haraka mtakula kibudu, kweli shehe happo hana haja ya kusema sijui kuna kibla au nini, hivyo hivyo anachinja, lakini yule mzee alikufa hakuwaachi hizo dawa, sasa hizo mila mila ndio hakuna
I: Mzee [Anonym] unadhani ni kwa sababu vijana hawataki kuzichukua hizo mila au wenyewe ndiyo hawakutaka kuwaachia vijana wao
R: Kwanza hizo mila zenyewe zilikuwa na taratibu ambayo haiendani na vijana, inawezekana wewe kwa mwezi unaoga mara moja, halafu hutakiwi ufue fue nguo sana itakate, halafu hutakiwi uchokoze ni ujiteteee, ukichokoza umevunja miko, ndio vitu kama hivyo, sasa vijana wa sasa hivi ukimpa hiyo dawa miko inaweza ikaisha siku moja
I: Ni watu gani walikuwa wakitengeneza njugha
R: Ni watu wanaitwa 'washanaa' yani ni kama unavyosema 'injinia' lakini kwa Kipare walikuwa walikuwa wanaitwa 'nimshanauo eshana njugha', yani anayetengeneza hizo njugha ambazo kwa Kisambaa ndio hizi 'mbughi'
I: Na walikuwa ni wa jinsia gani waliokuwa wanatengeneza hizo njugha
R: Ni wanaume tu
I: Wa kuanzia umri gani
R: Ni vijana tu ambaye mzee akikufundisha akishakukabidhi basi unafanya tu
I: Unaweza ukatambua ni vitu gani vilikuwa vikitumika kutengenezea njugha
R: Kuna vyuma vya zamani, mabati magumu na vingine vilikuwa vinatengenezwa kupitia vyuma ambavyo walikuwa wanapata kwenye mawe fulani, kwa mfano kuna mawe mpaka sasa hivi ukienda ukibomoa lile jiwe unapata jiwe wanaita jiwe la nyoka yale meusi, wanachoma kwenye moto inaiva wanagonga mpaka wanapata chuma cha kutengeneza njugha
I: Kwa hiyo ilikuwa ni chuma na kitu gani kingine, kwa mfano naona kuna mpini, huo mpini ni kitu gani
R: Huu mpini, walikuwa wanatengeneza mipini ya vyuma na kuna nyingine mipini ya mti, lakini mpini wa mti ni wa kukunjia tu huku juu kwa sababu inapasuliwa hivi, sasa kwa kwenye kukunja inatakiwa utumie nyundo ambayo ni nyepesi kidogo ili isije ikabonyea zaidi kuruhusu yale matumbo yake yafutuke hivi
I: Hivyo viti mlivyokuwa mnatengenezea njugha kwa miaka hiyo ya zamani viliendelea kuwa vinabadilika au ilikuwa ni miaka yote ni vifaa hivyo hivyo
R: Ilikuwa ni hivyo vinatumika havikubadilika mpaka inapotea
chanzo: Amani-Stade Project / Amani Field Research 2023, Interview No. 19
mwandishi: I: Mohamed Seif, R: Anonymous
Mtu
-
National Institute for Medical Research (NIMR)
(Mteja)
-
unknown actor
(wissenschaftlicheR BearbeiterIn)
Mahali