Wakati
2023-06-14
Maelezo
I: Sawa asante, tunaenda kwenye picha nyingine, kuna picha nyingine hapa imesajiliwa kwa namba 2018_18457_1, hebu tuambie hiki ni kitu gani
R: Hiki ni kibuyu ambacho kinawekewa vitu humo ndani kama vile maziwa, bwana anataka kusafiri anaweza akaweka hata uji humo akaenda zake, kinavaliwa hapa kwenye bega, hata mama amebeba mtoto anasafiri njiani amechoka akipumzika anampa mtoto vitu kupitia hii
I: Unaweza ukatuambia jina labda kulingana na kabila ambalo walikuwa wanatumia
R: 'Kibobo'
I: Hicho ni lugha gani
R: Kipare, lakini Kisambaa wanasema 'ntungo' au 'kinange'
I: Na kilikuwa kinapatikana mikoa gani hasa
R: Hiki kilikuwa kinalimwa sana kwenye miinuko ya Lushoto
I: Miinuko gani ya Lushoto
R: Kama vile Shume, Dare kule Malindi kwenye mnada, ukija hapa Lushoto mjini kule Mkuzi wanaita nkwai, na sehemu moja vilikuwa vinalimwa sana Mbwei, huku vinaanza kutengenezwa vinapambwa, hiki ni kitu kinavalishwa
I: Unaweza ukatuambia kimevalishwa nini hapo
R: Ni ngozi ambayo imetayarishwa lakini hasa wataalam wakuvitengeneza sana sana mpaka vinakuwa hivi ni Wambugu, wapo Mshangai na hapo Lushoto sehemu moja wanaita kwa Makame, na hapo kwa Makame ukitoka hapo unaenda sehemu ya Wambugu inaitwa Nesu
I: Kwa hiyo ilikuwa ni ngozi, kibuyu na kuna kama kamba
R: Hii kamba imesokotwa lakini sio kamba ya mkonge, kuna mti fulani huku wanaita 'sofokoo', lakini kule kwa Kipare unaitwa 'mnyambo' ndio unaosuka kamba hizi sio za mkonge
I: Na unaweza kutuambia matumizi yalikuwa yanatofautishwa baina ya jinsia labda wanaume na wanawake au ilikuwa ni jinsia moja tu ndio ilikuwa inatumia kibobo
R: Kwa wanawake ukimkuta na hiki ni Jumbe, kunaweza kukawa mwanamke mkubwa hapa kijijini watoto wote sisi tulipokuwa tu vijana, mnalazwa wote mle mwa Jumbe, hamna sijui kufikiria nini na nini, usiku mkiamka mnajisaidia haja ndogo hapo kwenye ng'ombe, wanawake wamelala huko na nyinyi, asubuhi mnaamka wote mko safi salama, sio sasa hivi...
Wote: Wanacheka
R: Sasa hivi akiwalaza hivyo hao watoto wa kike wanaweza wakahama usiku
Wote: Wanacheka
R: Hiki kinatumika kwenye vitu vingi, hata pombe, kuna pombe inaitwa 'yanzoki', nzoki ni asali, Kisambaa ni 'pombe ya wooki', sasa hiyo inatengenezwa maalum kwa ajili ya Jumbe inawekwa kwenye hiki anapelekewa Jumbe, basi anapiga kidogo anasema 'wajukuu wangu mmeingia mfunge mlango'...
Wote: Wanacheka
I: Kwa hiyo kwa wanawake ilikuwa ni kwa Majumbe
R: Ee
I: Na asilimia kubwa ilikuwa ni wanaume
R: Ni wanaume hao ndio ilikuwa ni kwa asilimia kubwa, unajua zamani wanawake walikuwa hawanyi pombe kama ilivyo hivi sasa, kwa sababu hivi sasa unaweza ukaenda baa ukamkuta mwanamke anapiga bia kuliko hata wewe na akakuambia karibu upate mbili tatu, na mwanamke wa zamani ukimkuta amelewa anapepesuka watakwenda kumhoji baba yake kwamba yule kamtibu, na anaweza akazuiwa asichanganyikane na watu wa nyumba nyingine wanawake wenzake kwamba ukoo ule sio mzuri wa kuoa, ukisikia tumemkuta mtoto wa fulani amelewa anapepesuka, yani watakuja wazee kuangalia anashida gani huyu au anaumwa, kwa mfano sasa hivi kuna biashara ya vipepeo, zamani ukionekana unacheza na kipepeo unaambiwa msicheze na ukoo ule kwa Kipare wanasema 'vegura pambarito' pambarito ni kipepeo, Wasambaa wanasema 'hoho', lakini zamani ukionekana unashika hiyo kitu mzee hawezi akasema nenda kaoe nyumba ile, unaambiwa 'aunga virishiravegura pambarito', umeshika kipepeo, lakini sasa hivi vipepeo ni hela
I: Mzee [anonymous], kibobo bado kinaendelea kutumika kwa sasa
R: Hapana, sasa hivi labda ukute sana huko ndani ndani unakuta kidogo kimetundikwa kama hivyo wazee walioachiwa mila, unaweza ukakikuta
I: Kwa hiyo umuhimu wake ilikuwa ni kwa sababu kinahusishwa na maswala ya mila
R: Ee, ila kilikuwa kina ladha nzuri sana kwa sababu pia kilikuwa ni kikombe cha kunywea maji, maji yakiwekwa kwenye mtungi hapo ukiyanywa utasema yametoka kwenye friji, mtungi ule kwa Kipare unaitwa 'mthambu', kwa Kisambaa 'igha', maji yakitoka humo ni haya yanayotoka kwenye friji, ila zamani mtindo kulikuwa mtindo wa kuambiwa chemsha maji haupo, sasa hivi unaambiwa maji yawekwe waterguard na nini..
I: Waliokuwa wanatengeneza hivyo vibobo walikuwa ni watu wa jinsia gani
R: Ni wanaume
I: Wa kuanzia umri gani
R: Ni umri wowote kwa sababu walioanzisha ni mababu, wakarithisha watoto wao, sasa hapo mzee na yeye akikuchunuka anakuambia kaa hapo uangalie vinavyofanywa, kwa hiyo unaweza ukamkuta mtu ana umri wa miaka ishirini lakini anatengeneza hivyo kwa kipindi hicho
I: Sawa, hicho kibobo unakiona jinsi kilivyo, kikiletwa sasa hivi wewe unakifahamu na matumizi yake, kinaweza kikauzwa sokoni shilingi ngapi
R: Zamani kilikuwa kinauzwa shilingi moja, lakini kwa mazingira ya kisasa kwa shilingi ya zamani kinaweza kikauzwa kwenye shilingi elfu tano
chanzo: Amani-Stade Project / Amani Field Research 2023, Interview No. 19
mwandishi: I: Mohamed Seif, R: Anonymous
Mtu
-
National Institute for Medical Research (NIMR)
(Mteja)
-
unknown actor
(wissenschaftlicheR BearbeiterIn)
Mahali